! Abstracts submission deadline extended to 31 Jan 2022

Mwito wa Ikisiri

Afrika na Binadamu: Maswali ya Kale, Tafakuri Bunifu Mpya

ASAA2022. Kongamano la nne linalofanyika kila baada ya miaka miwili. African Studies Association of Africa.
11–16 Aprili 2022. Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika ya Kusini.

ASAA2022: Dhana Fupi

Kuwa mwanadamu barani Afrika, kuwa mwafrika katika dunia ya leo kuna maana gani? Je, Afrika ina mchango gani kifikra wa kumjenga binadamu? Dhana ya binadamu inahatarishwa na mabadiliko tetereka kadri dunia inavyohama kutoka kile kinachosemekana kuwa ni kuzimu ya nadharia ya usasa na matokeo ya nadharia ya usasa-baadaye. Je, fikra kuu juu ya ubinadamu na/au kuwa Mwafrika zitadumu? Je, fikra juu ya nini maana ya kuwa binadamu na Mwafrika zitunzwe tunapoingia kwenye kipindi cha Anthropocene? Nini au nani ahesabike kuwa binadamu na/au Mwafrika? Wakati dhana za zama za Mwangaza zinapohojiwa na kukataliwa huku ukabila mamboleo kutoleta matokeo yaliyotarajiwa – ukitambulika kama mfumo wenye ulaghai na dhihaka – je, kuna fikra mbadala juu ya binadamu Afrika?

Mawazo kuhusu Afrika yanayumbayumba kutoka kuielezea kama sehemu iliyo na matarajio ya maendeleo na ambapo watu wake wana ubinadamu, na kuwa sehemu yenye majanga na kukata tamaa.Mara nyingi bara la Afrika hutajwa kama chimbuko la binadamu, mahali penye misingi ya falsafa ya ubinadamu, iliyojengeka kwenye falsafa za kuishi kijamii, kujali, ukarimu, kutegemeana, ambazo zina majina tofautitofauti ikiwemo teranga, ujamaa, ubuntu, na kadhalika. Bara hili bado linaonekana kuwa mahali penye matumaini ya kuwa na siku bora zijazo. Hata hivyo, taswira ya dunia juu ya bara hili kuwa sehemu yenye mateso, machungu na hali ya ukiwa, imeifanya kuonekana kuwa bara ambalo watu wake ni wakatili, hawajali utu, na walaghai. Kuongezeka kwa vifo eneo la Mediterranean, kushamiri kwa dhana ya utaifa unaojali ukabila, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, na kuongezeka kwa madai ya makundi ya watu au sehemu ya nchi inayotaka kujitoa kuwa nchi inayojitegemea, wizi wa kura katika uchaguzi wa kitaifa, kutofuata misingi ya katiba na haki, siasa za kibaguzi, serikali kandamizi, ukatili wa kijinsia, majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, majanga ya afya, kutelekezwa kwa jamii, hali ngumu ya uchumi, ni baadhi ya mambo yanayojirudiarudia katika mazungumzo yanayolihusu bara hili.

Matarajio yanayotajwa kufikiwa kwa kuwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, wingi wa wasomi wapya, mifumo mipya ya utawala na kuondokana na dhana za mipaka barani Afrika yameshindwa kufikiwa na kumkomboa, kumpa utu au kumjenga upya binadamu. Kumjadili binadamu ni jambo lenye uharaka na umuhimu, haswa tukizingatia kuwa tunaishi kwenye nyakati zenye majanga yaliyoikumba dunia nzima kama uviko-19, kutokujali wala kutoa kutoa kipaumbele kwa mchango wa sayansi katika kutatua majanga ya kimataifa, matarajio ya nadharia ya usasa-baadaye kuwa na hali ya usawa, haki za jamii, na mwisho wa historia ya ukatili, ubaguzi na umasikini kutofikiwa. Ni muhimu kutafakari namna ambavyo kuwa na mifumo ya demokrasia badala ya udikteta na ubabe wa kisiasa pamoja na kuongezeka kwa hali ya uvunjifu wa haki kunahusika na kuweka sawa epistemolojia za kiafrika ili kuwaza upya kama jamii ya kimataifa kuwa binadamu afananeje siku za usoni. Iwe kwenye fani ya kuzalisha fikra mpya, ufeministi, afya ya jamii, hisabati, fasihi, uhandisi, historia, biokemia, masomo ya siasa, kilimo, masomo ya dini na anthropolojia, au fani zingine, Afrika ilipo sasa ina fursa ya kuitengeneza upya dunia na kutoa masharti mapya ya jinsi tunavyopaswa kuenenda kwaajili ya vizazi vijavyo.

Ikiwa historia za hivi karibuni za ubaguzi wa rangi na ukoloni zimeonesha mkanganyiko uliopo kwenye kiini cha msimamo wa zama za mwangaza kudai kuwa tunaunganishwa na hali yetu ya asili ya kuwa binadamu, basi siasa za utambulisho za zama za sasa – zinazohusu misimamo katili, na wakati mwengine yenye athari za kimbari – imeharibu jitihada za kutengeneza mifumo ya kuishi katika hali ya amani, utu na kuheshimiana. Kuwa binadamu sio hali iliyo inaoeleweka kwa uwazi sana. Ndio maana kuna haja ya kuchunguza penye maswali, hali ya mvutano, na wakati mwengine mkanganyiko ulio wazi ulio kiini cha utambulisho wa binadamu. Je, tunatumia mbinu gani za kuwasilisha mawazo haya na mijadala hii, na tunatumiaje ujuzi huu katika maisha ya kila siku? Tunatofautishaje mambo haya na kuyaunganisha na historia, tamaduni, na uchumi mbalimbali?

Kongamano hili litachangia kujibu maswali ya wanazuoni yanayojirudiarudia kuhusu yale ambayo yanatuunganisha sisi wanadamu – huku tukitambua tofauti zetu – ambayo ni msingi wa kuchora kontua za siku zetu za usoni. Kuongezeka tena kwa jitihada za kupinga ubepari, ukoloni, mfumo dume, ubaguzi wa rangi, na kuunga mkono matumizi ya sayansi, haki ya utunzaji wa mifumo ya ikolojia na harakati zingine za kupigania haki za jamii zimehoji utatu wa hali ya binadamu kusimamia haki, hali ya binadamu kuwa mharibifu, utu wa binadamu. Je, Afrika inaweza kuleta mawazo gani mapya kujibu maswali na changamoto hizi, na tunatengenezaje nafasi za kutengeneza fikra mpya?

Tunaliona kongamano hili kama tamasha la mawazo, maabara ya nadharia na eneo la kufanya majaribio ya itikadi mbalimbali kuhusu Afrika na binadamu. Maandiko yatakayochaguliwa yatachapishwa kwenye mfululizo wa vitabu vya HUMA-ASAA “Encounters”. Likiwa limeandaliwa kwa ushirikiano wa HUMA – Taasisi ya Insia barani Afrika iliyopo Chuo Kikuu cha Cape Town, tuna lengo la kuwaleta wanataaluma mbalimbali – taaluma za sayansi ya jamii na insia (social sciences and humanities – SSH) na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) – ili wajadiliane juu ya namna bora za kuzalisha fikra mpya kuhusu Afrika na binadamu. Wanazuoni, wanaharakati, wasanii na watengeneza sera wenye uzoefu mbalimbali, kutoka vizazi tofauti, na taaluma yoyote ndani ya masomo sayansi ya jamii (SSH) na sayansi (STEM) wanaalikwa kuleta mapendekezo ya majopo yanayoendana na mada ya kongamano.

ASAA2022: Tarehe Muhimu

 • 01 Mei 2021: Mwito wa maombi ya majopo na warsha kabla ya kongamano
 • 11 Mei 2021: Mwanzo wa HUMA-ASAA “Kuhusu kuwa Binadamu Afrika: Midahalo ya Kiepistemolojia”
 • 30 Juni 2021: Kuwasilisha maombi ya majopo na warsha kabla ya kongamano
 • 11 Julai 2021: Kujulishwa kuwa maombi yamekubaliwa
 • 14 Julai 2021: Mwito wa ikisiri
 • 30 Sept 2021: Kuwasilisha ikisiri
 • 01 Nov 2021: Uandikishaji wa mapema ASAA2022
 • 14 Nov 2021: Kujulishwa kukubaliwa kwa ikisiri
 • 31 Jan 2022: Kufunga zoezi la uandikishaji wa mapema
 • 01 Feb 2022: Mwanzo wa zoezi la uandikishaji
 • 03–08 Apr 2022: Ziara kabla ya kongamano
 • 09–10 Apr 2022: Wahudhuriaji kuwasili kabla ya kongamano
 • 11–12 Apr 2022: Warsha na mikutano ya ASAA2022 kabla ya kongamano
 • 13 Apr 2022: Ufunguzi wa kongamano la ASAA2022 na mikutano ya pamoja
 • 14 Apr 2022: Midahalo ya kongamano la ASAA2022
 • 15–16 Apr 2022: Vipindi vya kongamano la ASAA2022 kufanyika sambamba
 • 17–22 Apr 2022: Ziara baada ya kongamano
 • 30 Mei 2022: Kuwasilisha dhana fupi kwaajili ya juzuu za mfululizo wa vitabu vya HUMA-ASAA “Encounters”
 • 30 Juni 2022: Kuwasilisha nakala ya kwanza ya makala kwaajili ya mfululizo wa “Encounters”
 • 01 Sept 2022: Kujulishwa kuwa nakala ya kwanza ya makala imekubaliwa kwaajili ya mfululizo wa “Encounters”
 • 30 Sept 2022: Kuwasilisha nakala ya mwisho ya makala kwaajili ya mfululizo wa “Encounters”
 • 01–30 Machi 2023: Uzinduzi wa mfululizo wa vitabu vya HUMA-ASAA “Encounters”

ASAA2022: Mwito wa Ikisiri

ASAA inawaomba wawasilishaji kuzingatia wigo wa mada ya kongamano zima katika makala watakazoziandaa. Tafadhali soma maelezo haya kwa makini, kisha bonyeza kitufye kitakachokuruhusu kutuma maombi yako. Kwakuwa tunapokea mawasilisho mengi mapendekezo ya ikisiri kwenye makongamano ya ASAA, Kamati ya Kongamano la ASAA2022 itahakikisha kuwa kuna mchakato wa upitiaji unaojali muda na unaofuata misingi ya haki kwa kufuata mifumo ya kimataifa ya mawasilisho hayo kupitiwa na watu usiowafahamu. Tunawategemea wanazuoni wenye uzoefu wa hali ya juu kutoka sehemu mbalimbali duniani katika kukamilisha mchakato huu.

Maamuzi ya Kamati ya Wanasayansi yatawekwa wazi Novemba 14, 2021. Usajili wa mapema utaanza Novemba 01, 2021.

Mawasilisho ya Mapendekezo ya Ikisiri

Masharti

 1. Mapendekezo ya ikisiri yasizidi maneno 250. Utahitaji kuambatanisha yafuatayo: a) Kichwa cha habari (yasizidi maneno 15), b) Muhtasari wa swali kuu na wazo la mjadala (yasizidi maneno 50), c) Ikisiri (yasizidi maneno 250), d) Wasifu yako (maneno 50)
 2. Mapendekezo ya ikisiri yanapaswa kutumwa kwa kutumia mfumo wa utumaji wa kongamano uliopo mtandaoni na sio kwa kutumia barua pepe.
 3. Waandishi wanaweza kuwasilisha mapendekezo yao kama mapendekezo ya ujumla au kwa kutuma moja kwa moja kwenye jopo wanalotaka kushiriki.
 4. Mchakato wa uhakiki ambapo mwombaji na mhakiki hawajuani utaendeshwa na Sekretarieti ya Kongamano chini ya uangalizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kisayansi/Mwenyekiti wa Kongamano.
 5. Mwenyekiti wa Kamati ya Kisayansi/Mwenyekiti wa Kongamano ni Kiongozi wa Kamati ya Kisayansi na ndiye mwenye maamuzi ya mwisho kuhusu mawasilisho ya ikisiri.
 6. Wajumbe wa Kamati ya Kisayansi ni wanazuoni wenye shahada ya uzamivu (PhD) au shahada ya kiwango cha mwisho katika nidhamu ya kitaaluma waliyomo na wenye uzoefu wa kufanya uhakiki na wataalamu wenza.
 7. Wajumbe wa Kamati ya Kisayansi ya Kimataifa watapitia kila ikisiri iliyowasilishwa kwa kufuata mfumo wa uhakiki ambapo mwombaji na mhakiki hawajuani, ndani ya wiki 2 baada ya makataa ya kupokea mapendekezo ya ikisiri.
 8. Majibu ya uhakiki wa ikisiri yatatumwa kwa mwandishi aliyewasilisha mapendekezo ndani ya wiki mbili baada ya makataa ya kupokea mapendekezo ya ikisiri (Vigezo vitazingatiwa iwapo kuna dharura).
 9. Arifa kuhusu kukubaliwa au kukataliwa kwa ikisiri zitatumwa kwa mwandishi aliyetuma zikiwa na maoni ya mhakiki panapohitajika,
 10. Iwapo kuna mapendekezo ya mhakiki, ikisiri iliyojumuisha mapendekezo hayo inapaswa kuwa imetumwa ndani ya wiki moja.
 11. Ikiwa ikisiri yako imekubaliwa, utatumiwa mwito wa kujisajili kuhudhuria Kongamano na kulipia ada ya uanachama wa ASAA ikiwa utataka kuwa mwanachama.
 12. Kila mwasilishaji wa makala anaweza kuwasilisha mara mbili (tafadhali tambua kuwa kuwa sehemu ya majadiliano ya vikundi vidogo “roundtable” inahesabika kuwa umeshiriki lakini sio kuwa umewasilisha mada). Mtu anaruhusiwa kuwa mwandishi-mwenza wa makala zaidi ya moja iwapo sio wao wanaowasilisha makala hayo.
 13. Viongozi wa vipindi (wanaosimamia ratiba) pamoja na wawasilishaji wa makala wanapaswa kujisajili kuwa wanachama wa ASAA na kulipia ada ya uanachama kabla ya kongamano kuanza. Siyo lazima kutimiza sharti hili wakati wa kuwasilisha mapendekezo ya ikisiri, lakini ni lazima walifuate sharti hili pale maombi yao yatakapokubaliwa,
 14. Wahudhuriaji wa kongamano, wakiwemo wanaochangia mada na wenyeviti, wanapaswa kujisali na kulipa ada ya usajili ili kuhudhuria kongamano.
 15. Makala zinazokidhi viwango vya Kamati ya Uhariri ya Kongamano zitapewa kipaumbele cha kujumuishwa kwenye mfululizo wa vitabu vya HUMA-ASAA Encounters. Mhariri atawasiliana na mwandishi wa makala iliyochaguliwa ili kujadili uwezekano wa kuichapisha ndani ya moja ya juzuu ya mfululizo wa vitabu hivyo.

Vigezo vya Mawasilisho Kukubaliwa

 1. ASAA2022 inaweza kuwa na waalikwa 500, hivyo kuwa na kama majopo 100.
 2. Kamati ya Kisayansi ndiyo yenye maamuzi ya kukubali mawasilisho ya ikisiri. Kukubaliwa huwenda ikawa kwa asilimia 50. Maamuzi hayo yatazingatia yafuatayo:
  • kuzingatia masharti yaliyoainishwa hapo juu
  • andiko linaloeleweka, lenye mawazo tangamano, linalofafanua fikra kwa weledi, na kuakisi ujuzi wa kitaaluma
  • Litaangaliwa kwa upekee: andiko linalozingatia mada ya kongamano, lengo/maudhui/maswali/wazo la mjadala, muundo wa makala, matumizi ya lugha sanifu, maadili yamefuatwa katika kufanya utafiti/methodolojia, majadiliano na hitimisho.
 3. Kamati ya Kisayansi itaangalia kwa upekee mifumo tofauti ya kitaaluma na mada zinazohusu SSH na STEM.

Vitu vya Kuzingatia katika Mawasilisho ya Mapendekezo ya Ikisiri

Mapendekezo yote yanapaswa kufanyika kwa kupitia fomu iliyopo mtandaoni. Mapendekezo yanapaswa kuwa na kichwa cha habari kisichozidi maneno 15, muhtasari wa swali kuu na wazo la mjadala usizidi maneno 80, ikisiri isizidi maneno 250), na wasifu wako usiozidi maneno 50. Mapendekezo ya ikisiri yasiwe na nukuu yoyote wala marejeo.

Baada ya kutuma mapendekezo, mwandishi aliyewasilisha mapendekezo (siyo waandishi wenza) atapokea uthibitisho kuwa mapendekezo yake yamefika kwa njia ya barua pepe. Iwapo hautapokea barua pepe hiyo ya uthibitisho, tafadhali bonyeza “Login” eneo la kushoto ili kuona kama wasilisho lako limeorodheshwa hapo. Ikiwa lipo, ina maana barua pepe ya uthibitisho imekwama na haikufanikiwa kukufikia. Na iwapo halipo hapo, ina maana inabidi uwasilishe pendekezo lako tena.

Mawasilisho yatawekewa alama ya kuonesha kuwa bado hayajapokelewa (“Pending”) au kuwa yamekwishapokelewa (“Submitted”) mpaka pale maamuzi ya Kamati ya Kisayansi yatakapowekwa wazi tarehe 14 Septemba, 2021. Siku hiyo, mawasilisho yatawekwa alama ya kuonesha kuwa yamekubaliwa (“Accepted”) au kukataliwa (“Rejected”), na waandaaji wa Kongamano watawasiliana na wawasilishaji kuwapa taarifa kwa njia ya barua pepe.

Urefu wa vipindi vya majopo

Kwa kuzingatia ufinyu wa rasilimali (mapendekezo ya majopo kuwa mengi kuliko muda uliopangwa) na shauku iliyowekwa wazi ya wanachama wengi kutaka kuhudhuria majopo mengi zaidi kuliko yale wanayohusika nayo moja kwa moja (aidha kwa kuyaongoza au kuwa wazungumzaji), majopo yatakayokuwepo kwenye ASAA2022 yatakuwa ya dakika 105. Majopo hayo hayatazidi vipindi viwili vinavyofuatana vya dakika 105 kila kimoja, na kila kimoja kitakuwa na makala zisizozidi tano. Hii itawezesha kuwa na vipindi vifupi vya majopo kwenye Kongamano na kwa wahudhuriaji na waliopendekeza makala kuhudhuria vipindi vingi zaidi. Kwahiyo, waongoza majopo (wanaosimamia ratiba) wataweza kuruhusu makala zisizozidi kumi kwa kila jopo. Hata hivyo, inaruhusiwa kuwa na makala nne kwa kipindi kimoja.

Wajibu wa waongoza majopo

Ni kazi ya kila muongoza jopo kuhakikisha kuwa wanajopo wanakidhi vigezo vya ASAA2022. Pia ni wajibu wao kuwasiliana na wanajopo kwa barua pepe: kuwataarifu kuhusu ratiba ya wanenaji (hata kama imewekwa wazi mtandaoni), kuwataarifu wamepangiwa muda kiasi gani, kuwakumbusha kufanya usajili (na kuwaelekeza wapi wanaweza kufanya hivyo), kuwataarifu kuhusu mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika na iwapo kuna wachangiaji watakaoongezeka, pamoja na taarifa nyingine yoyote inayohusiana na jopo. Wanajopo wakiomba udhuru kuwa hawataweza kushiriki, ni wajibu wa muongoza jopo kuwataarifu waandaaji wa Kongamano.

Muda wa Uwasilishaji

Wanaoongoza ratiba wana uhuru wa kupanga muda. Muongozo wa ASAA ni kuwa kila muwasilishaji anaweza kutumia si zaidi ya dakika 25 (kufanya uwasilishaji pamoja na kuwa na kipindi cha maswali/mjadala). Jambo la msingi ni kuheshimu kuwa kuna watu wamesafiri umbali mrefu kuweza kuja kuwa sehemu ya Kongamano na watahitaji muda wa kutosha kuwasilisha mawazo yao. Jopo la aina hilo litawekwa bayana kwenye ratiba, na makala zitakazokuwepo kwenye kipindi hicho. Ingawa waongoza majopo wanaweza kuamua kuunganisha vipindi, wanashauriwa kufuata ratiba ikiwa inawezekana.

Usambazaji wa Makala kabla ya Kongamano

ASAA haina sharti lolote juu ya hili. Hata hivyo, waongoza vipindi wengi hupenda kusambaza makala zilizokamilika kabla ya Kongamano. Ili kuratibu hili, na kupunguza wingi wa barua pepe, waandishi wanaweza kuweka makala zao wenyewe zikiwa kwenye nakala ya PDF kwenye mfumo ulioandaliwa na Kongamano mtandaoni. Mwandishi ana uamuzi wa kufanya hivyo au la.

Kuchapisha Makala

Makala ambazo zimekidhi viwango vya Kamati ya Uhariri ya Kongamano zina nafasi ya kujumuishwa kwenye machapisho ya mfululizo wa vitabu ya HUMA-ASAA “Encounters”. Mhariri atawasiliana na mwandishi wa makala iliyochaguliwa ili kujadili uwezekano wa kuichapisha ndani ya moja ya juzuu ya mfululizo wa vitabu hivyo.

Mawasiliano

Kwa taarifa zaidi, tafadhali tuandikie kupitia barua pepe hii: as-aa2022.org@uct.ac.za